Wizara ya Elimu nchini imewahakikisha wazazi na wanafunzi kwamba mitihani ya kitaifa itaendelea kama ilivyoratibiwa na maeneo yatakayotumika yakiwekwa ulinzi mkali ili kuzuia vurugu kutokea.
Kulingana na Mkurugenzi wa Elimu katika kaunti ya Mombasa Abdulkadir Kike, tayari mitihani ya kitaifa ya KCSE ya masomo ya mazungumzo ya lugha ya Kiarabu, Kifaransa, Kigerumani na lugha ishara yameanza kote nchini, huku usalama ukiimarishwa mashuleni.
Aidha, alisema kwamba juhudi zimeimarishwa na mitihani itaendelea bila ya pingamizi zozote, kwani baraza la mitihani nchini limejiandaa kikamilifu kushughulikia mitihani hiyo huku maafisa wa wizara ya elimu na idara mbalimbali za elimu wakijiandaa kusimamia mitihani hiyo iwapo walimu wataendelea kukaidi agizo la mahakama la kusitisha mgomo.
Akiongea na wanahabari afisi mwake mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Kike alisema kwamba baraza la mitihani litawajumuisha pia walimu wa shule za kibinafsi katika kusimamia mitihani hiyo, huku maafisa wa usalama wakituma katika vituo hivyo kuishika doria baada ya tetesi kuzuka kuwa walimu wanajama ya kuvuruga mitihani hiyo.
“Baraza la walimu limejiandaa kikamilifu likisaidiwa na maafisa wa idara ya elimu mashinani ili kuona kwamba mitihani ya kitaifa inafanyika bila changamoto zozote. Wazazi na wanafunzi wasiwe na hofu, usalama umeimarishwa kila mahali,” alisema Kike.
Haya yamejiri baada ya walimu kote nchini kushiriki mgomo ulioingia wiki yake ya tano sasa, na kuaahidi kusambaratisha shughuli zote za masomo iwapo serikali itazidi kukaidi walipa walimu nyongeza yao ya asilimia 50 hadi 60.
Vyama vya kutetea maslahi ya walimu nchini Knut na Kuppet vimeshikilia walimu hawatarudi shule hadi walipwe nyongeza yao pamoja na tume ya kuajiri walimu kuondoa kesi waliyoiwasilisha mahakamani ya kupinga nyongeza hiyo kabla ya walimu kufanya maamuzi.