Wakazi wa mtaa wa mabanda wa Langas, mjini Eldoret, wamesifia mpango wa serikali wa kuimarisha usalama katika makazi al maarufu Nyumba Kumi.
Wakizungumza siku ya Ijumaa, wakazi hao walisifu mpango huo kwa kusema kuwa umechangia kwa kina kukabiliana na visa vya kudorora kwa usalama katika mtaa huo.
“Tangu serikali ianze mpango huu wa Nyumba Kumi, tunalala vizuri hapa Langas. Kitambo wizi na mauaji ndio ulikuwa mtindo wa mtaa huu,” alisema Bw Charles Odenyo, mkazi.
Odenyo, ambaye pia ni mwenyekiti wa mpango huo mtaani humo, alisema ufanisi wa mpango huo mtaani humo umechangiwa na ushirikiano mwema kati ya utawala wa kaunti, idara ya polisi na wanasaisa kutoka katika mtaa huo.
Odenyo alisema mbali na kukabiliana na uhalifu, mpango huo umechangia kupunguza uraibu wa dawa za kulevya mtaani humo.
“Wakati Rais Uhuru Kenyatta alipotangaza vita dhidi ya pombe haramu, sisi hapa Langas tulikuwa tayari tumepiga hatua katika vita hivyo. Ni bayana kuwa mpango wa Nyumba Kumi umetuwezesha kukabiliana na dawa za kulevya,” aliongeza Odenyo.
Mshirikishi wa mpango huo mtaani humo Bw Annox Moturi alisema kijiji cha Kasarani kilikuwa miongoni mwa vijiji ambavyo vilikuwa vimeathiriwa pakubwa na ukosefu wa usalama, ambapo kwa sasa kiijiji hicho kimetulia kabisa kutokana na ushirikiano wa wenyeji kuboresha usalama kupitia kwa mpango huo.
“Kijiji hiki cha Kasarani kilikuwa ni ngome ya uhalifu ambapo hakuna mtu ambaye angependa kuishi hapa lakini kwa sasa, kila mtu anatamani kuishi hapa kutokana na mazingira nzuri ya usalama,” alisema Moturi.
Kamishna wa Kaunti ya Uasin Gishu Bw Abdi Hassan alisema kuwa wananchi katika mitaa ya mji wa Eldoret wamekumbatia mpango huo kutokana na matunda yake.
“Huu mpango umeturahisishia kazi kwani wananchi wanahusishwa katika udumishaji usalama katika makazi yao,” alisema Hassan.