Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wizi wa mifugo uliokita mizizi katika tarafa ya Kopere kwenye Kaunti Ndogo ya Muhoroni umepelekea wakazi kuanzisha msako.

Wiki moja iliyopita wakazi hao walionya kuchukua sheria mikononi mwao endapo washukiwa hawangekoma. Mnamo siku ya Jumamosi wananchi walionekana kufanya msako wa boma hadi boma kusaka ng'ombe aliyeibiwa kutoka kijiji cha Oseng'tet.

Ilidaiwa kuwa baada ya mifugo kuibwa hupelekewa wachuuzi wa mifugo ambao huchanganya mifugo wao pamoja na walioibiwa huku watu wakidhania kwamba wamenunuliwa.

Kiongozi wa mlango kumi kijijini hapo, Caleb Ogwang alitangaza kuwa yeyote atakayepatikana na hatia ya wizi wa mifugo katika eneo hilo lazima atakumbana na mkono wa sheria.

''Wananchi hawataendelea kupoteza mali yao huku watu wenye tamaa walio na nia mbaya wakijitajirisha kupitia mali ya wizi,'' alisema Ogwang wakati wa msako huo siku ya Jumamosi.

Aidha, Ogwang aliwataka wananchi kutochukua sheria mikononi mwao, akisema serikali ipo macho na kwamba itawanasa washukiwa wote.

Kuna visa kadhaa ambavyo vimeripotiwa majuma machache yaliyopita na majina ya washukiwa kunakiliwa. Sasa baadhi ya wafugaji eneo hilo hulazimika kukesha nje usiku ili kulinda mufugo yao huku wale walio na ng'ombe wachache wakiwajengea zizi karibu na nyumba za kuishi.