Share news tips with us here at Hivisasa

Mshukiwa wa wizi aliuawa kwa kushambuliwa na umati wa watu waliojawa na ghadhabu usiku wa kuamkia siku ya Alhamisi baada ya kufumaniwa katika zizi la mkazi mmoja katika eneo la Borabu, Kaunti ya Nyamira.

Akithibitisha kisa hicho siku ya Alhamisi, mkuu wa polisi Wilayani Borabu Kaunti ya Nyamira Athony Onyango aliwaomba wakazi wa kaunti hiyo kuungana pamoja na kushirikiana na maafisa wa polisi kwa kutoa habari wanazosijua kuhusu washukiwa wa wizi wa mifugo katika eneo hilo ili kutiwa mbaroni.

Mshukiwa huyo wa wizi aliyeuawa alifumaniwa katika zizi la mkaazi mmoja eneo la Borabu huku washukiwa wengine watatu wakifanikiwa kutoroka wakati mwenzao alikamatwa na kukatwa katwa kwa upanga na wakazi wa eneo hilo. Sasa tahadhari imetolewa katika eneo hilo kuwa yeyote atakayeshikwa kuhusika na wizi atatiwa mbaroni.

“Yeyote anayejua mshukiwa wa wizi katika eneo hili apashe habari katika kituo chochote cha polisi ili washukiwa hao watiwe mbaroni ili iwe funzo kwa wezi wengine wa mifugo,” alisema Onyango, mkuu wa polisi Wilayani Nyamira.

Wizi wa mifugo umekuwa ukishuhudiwa katika mpaka wa Kaunti ya Nyamira na wa Narok, kitendo ambacho kimeongezeka katika eneo hilo huku wezi wa mifugo kuonywa kuweka kando tabia ya wizi kila wakati, kwani siku zao zinahesabiwa na watakabiliwa  kisheria watakapofumaniwa.