Feri moja kati ya mbili zilizokuwa zikitoa huduma katika kivuko cha feri cha Likoni lilikwama na kusababisha msongamano mkubwa wa watu na magari siku ya Jumatatu.
Feri hiyo imekuwa ikihudumu kwenye kivuko hicho tangu siku ya Ijumaa baada ya mitambo ya feri nyingine kufeli kufanya kazi.
Baadhi ya wahudumu wa shirika hilo walisema kuwa kiwango cha maji kwenye ufuo huo wa maegesho kilipungua ghafla na kuiacha feri hiyo ikining’inia kwenye upande wa ardhi.
Mmoja wa mhudumu wa feri hiyo ya MV Nyayo, ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema kuwa kwa kawaida feri uhitaji kima kirefu cha maji ndio iweze kupakiza kwa njia ya rahisi.
Mhudumu huyo alisema kuwa feri hiyo ilijipata katika hali hiyo baada ya vipimo vya maji kushuka kwenye eneo la pili la Likoni kutoka Kisiwani na kuacha moja tu kuwahudumia watu na magari.
Hata hivyo, wenye magari ambao waliongea na mwandishi huyu walilaumu mamlaka ya feri kwa kuwa na visingizio badala ya kuleta feri za kutosha kuwahudumia wateja wao.
Simon Maina, ambaye ni dereva wa trela alisema kuwa hii si mara ya kwanza anashuhudia visa vya misongamano na kuhudumu kwa feri chache, na kuitaka serikali kuu pamoja na ile ya kaunti kuwajibika na kutatua tatizo hilo.