Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Huku mitihani ya kitaifa ya kidato cha nne KCSE ikianza hii leo, Wizara ya Elimu nchini imewahakikisha wazazi na wanafunzi usalama dhabaiti katika shule zote nchini.

Kulingana na Mkurugenzi wa Elimu katika kaunti ya Mombasa Abdulkadir Kike, tayari mitihani ya kitaifa ya KCSE ya masomo ya Sayansi ya kinyumbani na Sanaa yameanza kote nchini huku usalama ukimarishwa mashuleni.

Akiongea na wanahabari baada ya kuzitembelea shule za upili mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Kike alisema kwamba wizara ya elimu nchini imejianda kikamilifu kuhakisha kwamba mitihani hiyo inafanyika vyema, huku akisema kwamba wanatarajia matokea bora zaidi katika mitihani ya mwaka huu.

Aidha, amedokeza kuwa baraza kuu la mitihani nchini kwa ushirikiano na Wizara ya Elimu imeweka mikakati mwafaka ya kuhakikisha kwamba mitihani hiyo haikumbwi na chanagmoto zozote.

“Wizara ya Elimu kwa Ushirikiano na Baraza kuu la mitihani imeweka mikakati mwafaka ya kuhakikisha kwamba mitihani hiyo haikumbwi na chanagamoto za kuvurugwa na baadhi ya watu fulani. Maafisa wa usalama wanashika doria saa 24 katika shule zote mjini Mombasa,” alisema Kike.

Wakati uo huo, mkurugenzi huyo wa elimu katika kaunti ya Mombasa amewaonya wanafunzi dhidi ya kujihusisha na njia za udanganyifu akisema kwamba atakayepatikana atachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Tungependa kuwaonya wanafunzi dhidi ya kujihusisha na udanganyifu. Waachane na mambo hayo na kujibu maswali vile walifundishwa na walimu wao ili watoe matokea mazuri. Atakayepatikana akishiriki udanganyifu atachukuliwa hatua kali za kisheria,” alisema Kike.