Mvulana mmoja wa umri wa miaka nane kutoka eneo la Manga, Kaunti ya Nyamira aliaga dunia baada ya kuanguka ndani ya kisima cha maji.
Akitithibitisha kisa hicho siku ya Jumanne, naibu wa chifu wa lokesheni ya Morako, wilayani Manga, Jeremia Ogendi alisema mtoto huyo alikuwa anacheza na watoto wengine na kwa bahati mbaya akaanguka ndani ya kisima chenye futi nne.
Ogendi alisema wakazi walimsikia mtoto huyo akilia kutoka kwa kisima baada ya watoto waliokuwa naye kupiga kamsa na kujaribu kumwokoa.
Mtoto huyo alipelekwa katika hospitali ya Manga lakini madaktari wakasema tayari amefariki.
“Mtoto huyo alikuwa anacheza na watoto wengine karibu na kisima hiki cha maji na kwa bahati mbaya akaanguka humo ndani. Wakazi wa eneo hili walijaribu kumwokoa lakini alifariki alipokuwa akipelekwa hospitalini,” alisema Ogendi.
Wakazi wa eneo hilo walishangazwa na kisa hicho cha kufariki kwa mtoto mdogo ambaye hakutarajia kukutana na mauti.
Naibu chifu huyo aliwaomba wakazi walio na visima vya maji kuvifunika ili watoto wasije wakapoteza maisha kiholelaholela kwa kuanguka ndani.