Huku msako wa wanaotengeneza pombe haramu ukiendelea kote nchini, mwenyekiti wa shirika la kupambana na unywaji na matumizi ya dawa za kulevya, John Mututho amewataka machifu kuendelea mbele na msako huo.
Mwenyekiti huyo akiongea na machifu na manaibu wao katika eneo bunge la Nyaribari Chache kaunti ya Kisii siku ya Jumatano aliwaomba viongozi hao kuhakikisha kuwa lengo la kuangamiza pombe na dawa za kulevya umetimizwa ili kuwa na jamii iliyowajibika na kuwaokoa vijana ambao ndio wameathiriwa zaidi.
Mututho aliwaomba wale vijana, kina mama pamoja na wazee ambao wamechukua hatua ya kujiepusha na uraibu huo kuwa wazi na kuenda katika vituo vya urekebishaji mienendo ili kupewa msaada kama mojawapo ya hatua ya kuachana na matumizi ya pombe hiyo haramu.
Aliwapa changamoto viongozi wa kaunti hiyo ya Kisii kuwapa waathiriwa ushauri nasaha ambao utawapa matumaini ya kuendelea na maisha yao kama kawaida.
“Tuje pamoja kama jamii ili kuangamiza hizi sumu za pombe ambazo zinawamaliza watoto wetu na wazazi wetu, nawaomba viongozi wote mko apa kaza uzi kabisa ili tuliondoe jinamizi hili," Mututho alisihi.
Mkurugenzi huyo ameahidi kuendelea kupigana na unywaji pombe pamoja na matumizi ya dawa za kulevya, ambapo aliwashukuru wanajamii ambao wamekuwa katika mstari wa mbele kuona kuwa jamii inaishi bila ulevi na kuwataka kuendelea na juhudi hizo.