Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Shirika la kupambana na mihadarati na vileo nchini Nacada limeitaka serikali kuwatengea kima cha shilingi bilioni moja za kupambana na utumizi wa dawa za kulevya na vileo katika ukanda wa pwani.

Akiongea na wanabahari mjini Mombasa, baada ya kongamano la kujadili jinsi ya kusitisha kuenea kwa mihadarati eneo la pwani siku ya Alhamisi, mwenyekiti wa shirika hilo John Mututho, alisema kuwa fedha walizotengewa na serikali katika bajeti ya mwaka kamwe hazitoshi kushughulikia tatizo hilo na kuna haja ya serikali kuwaongezea fedha zaidi.

Kulingana na Mututho, shilingi milioni 160 walizotengewa na serikali ni kidogo mno ikilinganishwa na zoezi la kuwahamasisha jamii jinsi ya kukabiliana na mihadarati na vileo katika maeneo ya mashinani, kwani idadi kubwa ya waathiri wametorokea maeneo hayo.

“Fedha tulizotengewa na serikali ni kidogo mno na tungependa Rais Uhuru Kenyatta kutuongezea fedha hizo hasa eneo la pwani. Tunahitaji kuwa na kiasi cha shilingi bilioni moja kukabiliana na janga hilo hapa pwani,” alisema Mututho.

Alishinikiza jamii kuishi na waathiriwa vyema na kuwachukulia kama watu wengine ili kuwawezesha kuwa karibu nao na kuwasaidia kuwaondoa katika changamoto hizo, kwa kuwapeleka katika vituo vya kurekebisha tabia na kusitisha kuenea kwa mihadarati.

“Vijana waliyoathiri ni jamaa zetu. Sioni haja ya kuwatenga na kuwa dhulumu kwani hatua hiyo kamwe haitasaidia kusitisha kuenea kwa mihadarati. Ni lazima tuwachukulie vizuri na kuwapeleke kwa vituo vya matibabu na walanguzi wakuu watiwe nguvuni na kufungwa maisha,” aliongeza Mututho.

Aidha, amewataka magavana wa kaunti zote za pwani kuanza zoezi la kuzifunga baa ndogo pamoja na kuzinyima liseni ili kusitisha kuenea kwa utumizi wa dawa za kulevya na vileo.

Alisema kuwa hatua hiyo itainusuru idadi kubwa ya vijana wadogo waliyoathiriwa na utumizi wa mihadarati na vileo.

Mututho alishinikiza Rais Uhuru Kenyatta kuongezea pesa shirika hilo kwani zoezi la kuihamasisha jamii mashinani pamoja na kupambana na watumizi na walanguzi wa mihadarati katika ukanda wa pwani unahitaji fedha za kutosha.

Kauli ya wakurugenzi wa shirika hilo imejiri siku chache tu baada ya Rais Uhuru kenyatta kutangaza vita dhidi ya dawa za kuelvya na vileo katika ukanda wa pwani.