Wakazi wa wadi ya Kisii ya kati watanufaika pakubwa na mradi wa barabara na maji baada ya mwakilishi wao kutangaza kuwa ataendeleza miradi hiyo kati wadi hiyo.
Akiongea siku ya Jumapili na wakazi katika eneo la Kiamabundu wadi ya Kisii ya Kati, mwakilishi wa wadi hiyo Alfred Monyenye alisema kuwa serikali ya kaunti ya Kisii imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa barabara katika wadi hiyo zimefunguliwa ili kuinua viwango vya uchukuzi katika eneo hilo.
“Tutafungua barabara zaidi katika wadi hii ili kuhakikisha kuwa sekta ya uchukuzi imenawiri pakubwa kwa kuwa wengi wetu ni wafanybiashara na ni lazima tutumie barabara hizo kufanya bishara hizo,” alisema Monyenye.
Monyenye aliwaomba wakazi kushirikiana naye ili kutambua barabara ambazo zinahitaji kukarabatiwa.
“Nawaomba tushirikiane ili tutambue baadhi ya barabara zinazohitajika kufunguliwa ili sekta ya uchukuzi inawiri,” alisema Monyenye.
Mwakilishi huyo alisema kuwa serikali ya kaunti pia imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa kila boma itakuwa na maji, huku akisema kuwa atahakikisha kuwa mito imekarabatiwa ili wakazi wapate maji safi.
Monyenye alisema kuwa mto wa Kenonga utakarabatiwa na kutengenezwa kwa njia ya kisasa ili kuwafaidi wakazi wa eneo hilo.
Aidha, aliwaomba wakazi kushirikiana na ofisi yake ili kuhakikisha kuwa viwango vya maendeleo vimenawiri pakubwa katika eneo hilo.