Machifu wote katika wadi ya Esinse iliyoko eneo bunge la Mugirango Kaskazini kaunti ya Nyamira, wameombwa kutosambaza habari za uongo kuwa pesa za maendeleo za wadi hiyo zilitumika vibaya.
Akizungumza siku ya Jumanne na waandishi wa habari katika mji wa Nyamira, mwakilishi wa wadi hiyo ya Esinse, Teresa Nyangaa, alisema machifu husambaza habari kuwa pesa za maendeleo katika wadi hiyo zilitumikwa vibaya.
Mwakilishi huyo alikanusha madai hayo na kusema pesa hizo zilitumika vizuri kulingana na ratiba ya wadi hiyo.
“Naomba machifu na watu wote wa wadi yangu haswa wale wako na maoni ya maendeleo waungane nami tusaidie wadi ya Esinse iendelee mbele kimaendeleo,”alisema Nyaanga.
“Haya mambo ambayo husambazwa hapa na pale kuwa pesa zilitumikwa vibaya na kulikuwa na ufisadi si ya ukweli. Kufanya maendeleo ni kushirikiana pamoja lakini haya mengine si ya ukweli,”aliongeza Nyaanga.
Aidha, aliomba machifu na manaibu wao na hata baadhi ya watu wanaosambaza habari hizo ambazo zinahusu utumizi mbaya wa pesa kufanya kazi yao husika na kuweka kando njama ya kuharibia watu jina.
Wakati huo huo, mwakilishi huyo alisema amepanga kuwa na kikao na watu wa wadi yake ili kuwaelezea jinsi pesa hizo zilivyotumika.
“Nitawambia watu wangu siku tutakayokutana nao nikiandamana na waziri wa pesa katika kaunti ya Nyamira, waziri wa barabara na waziri wa miradi yote ya maendeleo ili tuwaelezee jinsi pesa zilitumika katika wadi yangu,” alisema Nyaanga.
“Hakuna wizi wa pesa maana kuna tume ya kupambana na ufisadi. Naomba watu kuacha kuniaribia jina,” aliongeza Nyaanga.