Mwalimu wa dini aliyeshukiwa kulawiti wavulana 15 mjini Elburgon, Nakuru alifikishwa mbele ya mahakama ya Molo siku ya Jumatano kujibu mashtaka hayo.
David Mugo, mwenye umri wa miaka 35, anakabiliwa na shtaka la kuwalawiti wavulana hao wenye umri kati ya miaka nane na 13 kwenye maeneo ya Kasarani mjini Elburgon.
Hata hivyo, Mugo alikana mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkaazi James Wanyanga.
Mahakama ilitoa amri kuwa Mugo awekwe kwenye rumande katika Kituo cha polisi cha Elburgon mpaka maafisa wa polisi watakapomaliza uchunguzi.
Hakimu Wanyanga aliwaonya wakazi dhidhi ya kuingilia uchunguzi unaofanywa na maafisa wa polisi.
“Mahakama haiwezi kuvumilia wakazi wanaotishia kumdhuru mshukiwa kama walivyojaribu kufanya kwenye Hospitali ya Nyayo mjini Elburgon, ambako waathiriwa walitibiwa. Wacheni sheria ifuatwe kwa utaratibu. Kama alifanya kitendo hicho, basi atajipata mikononi mwa sheria kwani polisi tayari wanaendelea na uchunguzi,” alisema Wanyanga.
Polisi walikuwa na wakati mgumu wa kudhibiti wakazi waliotaka kumvamia mshukiwa huyo siku ya Jumanne walipokuwa wakisafirisha mshukiwa huyo kwenye hospitali ili kuchunguza hali yake ya afya.