Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Msimamizi mkuu wa shule ya watoto wasioongea na kuelewa (Pupils with Autistic Condition) katika shule ya msingi ya Kisii ameomba serikali ya kaunti ya Kisii na wahisani kutoa msaada wa kifedha ili kuwafaa kusafirisha watoto hao kutoka nyumbani hadi shuleni na kurudi makwao.

Akizungumza siku ya Ijumaa katika afisi yake, Pamela Kemuma, alisimulia baadhi ya masaibu na changamoto nyingi wanakumbana nazo wanaposhughulikia watoto hao shuleni, huku akisema kuwa baadhi yao hususia kula.

Kemuma alisema kuwa wazazi wengi wa watoto hao ni fukara sana kiasi kwamba hawawezi kupata nauli ya kuwasafirisha watoto wao kila siku kuja shuleni, hali ambayo ametaka serikali ya kaunti ya Kisii kuingilia kwa dharura ambapo alitaka wanunuliwe gari la kuwasafirisha watoto hao au mtu yeyote ajitolee kuwabeba watoto hao kuwapelea shule.

Hata hivyo, Kemuma hakusita kuwashukuru wahisani ambao wamekuwa wakiwasaidia na kuwataka wazazi pamoja na jamii kwa jumla kuwakumbatia watoto walio na ulemavu huo kama njia mojawapo ya kuwaonyesha upendo.

Kwingineko, mwalimu mkuu wa shule hiyo ya msingi ya Kisii, Bi Grace Nyamweya na naibu wake Julias Ocharo wameongezea uzito kkwa suala hilo, huku wakiwataka viongozi kutoka eneo la Kisii na kaunti kwa jumla kuwafadhili katika ujenzi wa jumba la malazi kwa wanafunzi hao kwani itakuwa rahisi watoto hao kulelewa shuleni ili angalau kuwapa wazazi nafasi ya kupumua na kuendelea katika shughuli nyingine za kujenga nchi.