Mwanafunzi wa mwaka wa nne wa chuo kikuu cha Egerton anasakwa na polisi baada ya kudaiwa kumuua msichana mmoja mwendo wa saa nne usiku siku ya Alhamisi.
Kisa hicho kinasemekana kilitendeka katika mtaa wa 'Railways station area', mkabala na hospitali kuu ya mkoa wa bonde la ufa, PGH.
Kwa mujibu wa OCPD wa Nakuru Bernard Kioko, mwanafunzi huyo kwa jina la Samuel Muhia anayesomea taaluma ya utabibu, alikwenda na msichana huyo mwenye umri wa makamo nyumbani mwake na kudaiwa kutekeleza mauaji hayo.
OCPD kioko alisema kuwa huenda Muhia alitofautiana na msichana huyo ambaye jina lake halijabainika, na kumnyonga na kisha kutoweka usiku huo.
“Marehemu alipatikana na polisi akiwa kitandani humo, huku nyaya za umeme zikiwa zimefungwa shingoni mwake,” alisema Kioko.
Kioko alisema kuwa baada ya polisi kufika katika chumba hicho, waliupiga mwili wa marehemu picha na kisha kuuondoa na kuupeleka katika Ufuo wa Kaunti ya Nakuru kwa upasuaji.
Kioko alisema polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi wa kumsaka mwanafunzi huyo huku akitoa wito kwa yeyote aliye na habari kuhusu alikotorokea mwanafunzi huyo, kuripoti katika kituo cha polisi kilicho karibu.