Share news tips with us here at Hivisasa

Mwanamume wa umri wa miaka 38 kutoka kijiji cha Nyabigena, wilayani Gucha Kusini, amepoteza maisha yake baada ya kuangukiwa na udongo.

Inaripotiwa kuwa udongo ulianguka kwenye nyumba ya mwanamume huyo, Mauti Seme, na kumuua papo hapo kufuatia mvua inayonyesha katika eneo hilo.

Akithibitisha kisa hicho siku ya Jumanne, Mkuu wa polisi wilayani Gucha Kusini, Moses Kanyi, alisema kifo hicho kilisababishwa na mvua nyingi iliyosababisha udongo kuanguka.

Mkuu huyo wa polisi aliomba wakazi kuwa makini wakati wa mvua ya El Nino na kuwaonya dhidi ya kujikinga chini ya miti ili kuzuia maafa.

“Naomba wakazi wawe makini mvua inapoendelea kunyesha. Leo ni siku ya pili tangu mvua kubwa kuanza kunyesha lakini watu wanne tayari wamepoteza maisha yao kupitia visa vilivyosababishwa na mvua hiyo,” alisema Kanyi.

Watu watatu kutoka wilayani Kenyenya eneo bunge la Bomachoge Chache, walipoteza maisha yao kwa kupigwa na radi siku ya Jumatatu.