Mwanamume mmoja Alhamisi asubuhi alifikishwa kwenye mahakama moja mjini Nakuru kujibu shtaka la kumnajisi mtoto mwenye umri wa miaka 14 katika eneo la Cyder Lodge katika Wilaya ya Nakuru Kaskazini.
Moses Njau alidaiwa kutenda kitendo hicho cha kinyama mnamo tarehe mwezi Mei 14 mwaka uliopita. Kesi hiyo ilisikizwa chini ya Hakimu Mkazi wa Nakuru Judicaster Nthuku.
Nyanyake mtoto mwathiriwa, ambaye pia ni mkulima alielezea mahakama kuwa alingoja kwa muda mwingi siku hiyo jioni ili mtoto huyo ambaye alikuwa darasa la nane arejee nyumbani ila matumaini yake ya kumuona yaliambulia patupu.
Aliambia mahakama kuwa ilimbidi atafute usaidizi wa majirani ili kubaini alipokuwa mtoto huyo ndiposa katika majira ya saa tatu usiku, akafahamishwa na mmoja wao kuwa mtoto huyo alikuwa nyumbani mwa mshtakiwa.
Mmoja wa majirani hao alimpeleka katika kituo cha polisi kuripoti tukio hilo na ndipo maafisa wa usalama wakaelekea hadi nyumbani mwa mtuhumiwa walikompata mtoto huyo.
Njau alikamatwa na maafisa hao huku mtoto huyo alipelekwa katika Hospitali ya Maili Kumi alikopata matibabu.
"Mmoja wa majirani alinishauri twende katika kituo cha polisi kuripoti tukio hilo, mtuhumiwa alikamatwa nyumbani kwake na mtoto huyo ambaye nilimpeleka hospitali ya Maili Kumi kwa matibabu," alisema nyanyake mtoto.
Kesi hiyo itasikizwa tena mwezi Oktoba tarehe tano mwaka huu huku mashahidi zaidi wakitarajiwa kutoa ushahidi wao dhidi ya mtuhumiwa.