Share news tips with us here at Hivisasa

Mwanamume wa umri wa miaka 32 amefungwa miaka tano gerezani baada ya kupatikana na hatia ya kuiba mifugo ya wakulima katika eneo la Ndumberi. 

Joseph Kirima alihukumiwa kifungo hicho baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa ng'ombe wawili wa maziwa na mbuzi mmoja mnamo Juni 19, 2015 katika eneo la Ndumberi kaunti ya Kiambu kisha kuwauza kwa mkulima mmoja eneo la Githunguri.

Hakimu Diana Mochache alitoa uamuzi wa kesi hiyo siku ya Ijumaa katika korti moja la Kiambu baada ya upande wa mashtaka kuleta washahidi wawili kutoa ushahidi wao.

Mshaidi wa kwanza alikuwa Richard Kimani ambaye ni mkulima katika eneo la Githunguri ambaye aliuziwa mifugo hao.

Kimani alielezea kwamba mnamo tarehe 20 wezi jana, Kirima alienda nyumbani kwake akiwa na haja ya pesa na alikuwa anauza mifugo hao kwa bei ya chini.

Alipomuuliza alikotoa mifugo hao, alisema kwamba mifugo hao walikuwa wake na alikuwa anahitaji pesa kwa dharura kwani alikuwa anataka kumaliza ujenzi wa nyumba yake.

Alisema kwamba alikubali kwa kuwa alimwamini kama mwandani wake wa kale na kununua mifugo hao wote kwa elfu 20.

Alikiri kwamba baada ya muda wa wiki mbili, polisi wakiandamana na mlalamishi walikuja hadi nyumbani kwake na kumhoji kuhusu mifugo hao.

Alisema kwamba alishikwa kama mshukiwa wa kwanza na ikabidi ampigie mshukiwa kwa kuwa yeye ndiye aliye muuzia mifugo hao.

Mshahidi wa pili alikuwa mkulima katika eneo la Njonu ambaye alikiri kwamba mshukiwa alikuwa amekusudia kumuuzia mifugo hao.

Alisema kwamba alidinda kununua kwa kuwa alishuku mshukiwa kwa wasiwasi aliyokuwa nao kwa kuwa alikuwa anataka kuwauza mifugo hao kwa bei yoyote.

Kirima alipewa nafasi ya kujitetea kabla ya hukumu na alisema kwamba alikuwa na jamii ambayo ilikuwa ikimtegemea akiwemo nyanya yake ambaye anaugua na yeye ndiye anashughulikia matibabu yake.

Alikiri kwamba alikuwa amekosea na hatorudia kosa hilo tena. 

Hakimu Mochache alimhukumu kifungo cha miaka tano gerezani na kumpa siku kumi na nne za kukata rufaa.