Mwanaume mwenye umri wa miaka 25 Jumanne alifikishwa mbele ya mahakama ya Kisumu kujibu shtaka la wizi wa mabavu.
Tobias Okinyi alikana madai hayo mbele ya Hakimu Mkuu wa Kisumu Lucy Gitari kwa kosa analoshtumiwa kutekeleza mnamo mwezi Juni tarehe 29 mwaka huu mjini Kisumu.
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, mshukiwa ambaye ni mkazi wa mtaa wa Manyatta iliyoko jijini Kisumu, alimvamia Joseph Obonyo ambaye ni muajiri wake usiku wa mwezi Juni tarehe 29.
Kiongozi wa mashtaka aliongezea kuwa wakati wa uvamizi huo, Obonyo alikua nuyumbani mwake pekee yake huku mshukiwa alikua na watu wengine wawili ambao bado wapo mafichoni.
Inadaiwa kuwa mshtakiwa na wenzake waliiba mali ya thamani ya Sh200,000, ikijumuisha simu ya rununu, runinga, tarakilishi na dekoda tatu.
Obonyo ambaye ni mkazi wa Milimani Kisumu aliweza kuokolewa na majirani wake ambao waliamshwa na vurugu iliyokua ikiendelea nyumbani mwake.
Usaidizi ulipowasili, Okinyi na wenzake walikuwa washatoweka na mali hiyo ya wizi. Polisi waliarifiwa kuhusu kisa kilichotendeka na uchunguzi ukaanzishwa mara moja huku mshukiwa Okinyi akiwa mshukiwa mkuu kwani mwajiri wake Obonyo aliweza kumtambua.
Okinyi alikamatwa mnamo mwezi Julai tarehe 3 mwaka huu mtaani Kondele, Kisumu. Uvamizi huo ulimuacha mlalamishi Obonyo na majeraha yaliyompelekea kulazwa hospitalini kwa mda wa siku tatu.
Hakimu Gitari alimuachilia mshukiwa Okinyi kwa thamani ya Sh20,000 huku kesi hiyo ikihairishwa hadi mwezi Agosti tarehe 22 mwaka huu.