Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Msanii kutoka Kaunti ya Kisii Nyang'wara Mosioma anayefahamika kwa lakabu ya kisanii kama Embarambamba, amewataka wanamuziki wenzake kutumia vizuri pesa wanazopata na kujiepusha na anasa.

Msanii huyo anayeimba nyimbo za mtindo wa benga aliongea na Mwandishi huyu mjini Kisii, katika makao makuu ya jumuia ya wakulima wa kahawa alipokuwa katika harakati za kujiandaa katika tamasha la kuburudisha wakazi wa eneo hilo siku ya Jumatano kwenye taasisi ya mafunzo ya wakulima al maarufu KFTC.

Embarambamba alitaja madai ya baadhi ya wasanii ambao wamekuwa wakiwalaumu mapromota wao kwa masaibu wanayopitia kuwa ni kisingizio tu, akisema kuwa hata yeye alianzia kuimba katika hafla nyingi zingene hakulipwa hata, lakini alijikaza hadi kufikia kiwango alicho kwa sasa ambapo anajivunia kufaidi pakubwa kutokana na muziki.

Mwanamuziki huyo aliwasihi wasanii wenzake kupunguza starehe na uraibu wa kutumia mihadarati pamoja na unywaji pombe ambao alitaja kuwa chanzo cha wanamuziki na jamii kwa jumla kukosa kupiga hatua katika maisha.

Kwa upande mwingine Embarawasinga anavyopenda kujiita mara nyingi, aliwasuta baadhi ya watengezaji nyimbo za wasanii al maarufu Producers ambao wamekuwa katika mazoea ya kutumia wasanii vibaya kwa kuwanyonya jasho huku wakiwalipa hela kidogo ilhali wao ujigawia pato kubwa na kusababisha wengine kuachana na mambo ya muziki.

Aidha, aliwataka wasanii kutoka eneo la Gusii kwa jumla kuiga mifano ya baadhi ya bendi pamoja na wanamuziki binafsi ambao wamepiga hatua kimaisha kupitia muziki akitoa mfano wa bendi kama Bana Sungusia, Bonyakoni pamoja nay yeye mwenyewe na kuwasihi wenzake kufanya muziki kama biashara na kujiepusha na starehe zisizo na faida kwao.