Mwanasiasa aliyewania kiti cha ubunge cha Kitutu Chache Kaskazini James Atandi amesema hafurahishwi jinsi pesa za hazina ya Uwezo Fund zinakabidhiwa watu wa eneo hilo.
Akizungumza mnamo siku ya Alhamisi katika lokesheni ya Mwamonari, eneo bunge la Kitutu Chache, mwanasiasa huyo aliomba uwazi kutekelezwa katika hazina hiyo ili vijana wa umri mdogo wapate pesa hizo pamoja na akina mama ili kujiendeleza na kujiimarisha kimaisha.
Aidha, aliomba vijana wote wa eneo bunge hilo kujiandikisha kwa vikundi ili wakabidhiwe pesa hizo na kuinua uchumi wan nchi ya Kenya.
“Pesa za uwezo zilikuja kwa maeneo bunge ili watu wafaidike nazo kwa kuzikopa ili kufanyia biashara, lakini kuna masuala hufanyiwa kichini chini kuhusu hazina hiyo ambayo si ya kufurahisha, ninawaomba vijana kujitokeza kwa wingi mpate hizo pesa,” alisema Atandi.
Kwa upande mwingine, wakaazi wa eneo hilo walionekana kuunga mkono mwanasiasa huyo kwa kudai kuwa pesa hizo huwa hazijulikani vle zinatumika.
“Huwa tunasikia kuwa serikari ya kitaifa ilianzisha hazina ya Uwezo Fund kwa kila eneo bunge lakini kama mimi nilisikia mara moja na sijui ziko wapi ili nipatiwe nifanyie majukumu ya ubadilishanaji,” alihoji Victor Ogari, mkaazi.
“Mie naomba tuambiwe jinsi ya kuzipata pesa hizo ili tukabidhiwe tufanyie biashara na tujijenge kimaisha,”alidokeza Beatrice Bibao, mkaazi mwingine.