Mwanamme mmoja siku ya Jumatano alifikishwa mbele ya mahakama ya Nakuru kwa shtaka la mauaji.
Mshtakiwa huyo kwa jina Stephene Koigi alishukiwa kumuua afisa wa polisi kwa jina Abraham Njenga Kamau kwa kumdunga kisu katika kijiji cha Masaita eneo la Londiani, Kaunti ya Nakuru.
Mshtakiwa anatuhumiwa kwa madai ya kutekeleza mauaji hayo mnamo tarehe Disemba 25 mwaka wa 2013.
Marehemu ambaye alikuwa amerejea nyumbani kutoka kazini saa 12:00 jioni akiandamana na mwana dada mmoja, ilidaiwa kufumaniwa na mshtakiwa mwendo wa saa tano unusu usiku kwa madai kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na binti huyo Betrice Waithera aliyekuwa mkewe Stephene Koigi ingawa walikuwa wametengana kwa muda.
Waithera ambaye alifanikiwa kutoroka ingawa kwa majeraha ya kisu mgongoni aliweza kuwaita majirani na kumpigia simu Inspekta wa polisi, Aden Msumba na kumweleza kilichotokea usiku huo.
Iliwachukua maafisa wa polisi siku kadhaa kumkamata mshtakiwa huyo amabaye alienda mfichoni baada ya kutekeleza kitendo hicho cha unyama. Waithera naye alipelekwa hospitali ya Molo kuuguza majeraha aliyoyapata.
Akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkuu Mary Otindo, Waithera alieleza mahakama hiyo jinsi mshukiwa huyo alivyowavamia kwa kisu mara kadaa na kumuua marehemu papo hapo, madai ambayo yaliungwa mkono na daktari ambaye aliufanyia ukaguzi mwilini mwa marehemu huku akiongeza kwamba sehemu kadhaa za mwili zilikuwa hazipatikani.
Kesi hiyo itaendelea mwezi Novemba 19 mwaka huu.