Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi ameshutumia vikali hatua ya maafisa wa polisi na vijana waliohusika katika ubomozi wa nyumba za wakazi wa eneo la Dunga Unuse katika eneo bunge hilo akisema kwamba ni ukiuakaji wa katiba ya nchi.

Kulingana na Mwinyi, kuna baadhi ya maafisa tawala wanashirikiana na mwabwenyenye kuwafurusha wakazi hao katika ardhi hiyo wanayomiliki tangu jadi ili kuekeza miradi yao ya kujinufaisha wenyewe.

Akizungumza katika eneo la Dunga unuse siku ya Jumatano, Mwinyi alisema kwamba lazima hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika hata baada ya wakazi hao kuzijenga upya nyumba hizo.

“Hatua ya ubomoaji wa nyumba za wakazi wetu ni ukiukaji mkubwa wa katiba ya nchi na lazima hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika. Serikali inafaa kuzingatia haki za mwananchi wa kawaida lakini sio kuwaacha maafisa wake tawala kushirikiana na mwabwenyenye na kuwafurusha wakazi,” alisema.

Aidha aliongezea kwamba ataijumuisha serikali ya kaunti ya Mombasa katika kuwatetea wakazi hao kumiliki ardhi hiyo, kwani serikali inafaa kuwatengea mahali maalum pa kuishi iwapo inalenga kuwauzia mabwenyewe ardhi hiyo ili kuekeza, huku akiwahimiza wakazi hao kamwe kutoondoka eneo hilo.

Zaidi ya familia 300 zimebomolewa nyumba zao na kuachwa bila makao licha ya viongozi hao kutoa agizo la shughuli hiyo kusitshwa na kuitisha mazungumzo kutokana na ardhi hiyo kuwa ya umma.