Naibu wa Gavana wa Kaunti ya Nakuru Joseph Ruto amelaani vikali kumwagwa kwa pombe haramu katika maeneo ya barabara katikati mwa mji wa Nakuru.
Akiongea katika uzinduzi wa Link Therapeutic Centre katika eneo la Njoro kwa niaba ya Gavana wa Nakuru Kinuthia Mbugua, Ruto alilaani uharibifu wa mali na kuingizwa siasa kwenye operesheni hiyo ambayo alisema imeharibu mazingira kwa umwagaji wa pombe kiholela mjini humo.
Naibu gavana huyo alisema kuna njia nyingi tofauti viongozi wanaweza kutoa hisia zao na wala sio kujihusisha kwa vitendo vya uharibifu ambavyo viliweza kusababisha msongamano mkubwa wa magari mjini Nakuru na hivyo kuwaathiri wananchi.
Alihakikisha kuwa kama serikali ya kaunti, wanaiunga mkono vilivyo operesheni ya kubiliana na pombe haramu lakini haifai kutumiwa kama kigezo cha mapambano ya kisiasa akiongeza kuwa shughuli hiyo inapaswa kutekelezwa kufuatia sheria.
Ruto pia alisema waliotekeleza shughuli hiyo ya kumwaga pombe katika barabara moja mjini Nakuru wanapaswa kufahamu kuwa hawakufanya jambo jema na wanarudisha serikali ya kaunti nyuma kimaendeleo kwani wametumia muda mwingi kuboresha mji huo.
Pia aliongeza kuwa vitendo kama hivyo vitawafukuza wawekezaji waliomo Nakuru, jambo ambalo alisema litarudisha kaunti hiyo nyuma kimaendeleo na kuwa viongozi waepuke siasa duni zilizopitwa na wakati.
"Vitendo kama hivyo tulivyovishuhudia mjini Nakuru vinaturudisha nyuma kimaendeleo kwani vinaweza pelekea wawekezaji watutoroke," alisema Naibu Gavana Ruto.