Serikali ya kitaifa imeombwa kuwalipa walimu nyongeza yao ya mishahara ili kusitiza mgomo ambao unaenedelea kushuhudiwa nchini.
Akizungumza siku ya Alhamisi katika eneo la Manga, Kaunti ya Nyamira, Katibu mkuu katika chama cha ODM Ababu Namwamba alisema serikali ina pesa za kutosha ambazo zinastahili kutumika kuwalipa walimu badala ya kususia kuwalipa nyongeza yao ya mshahara.
“Mimi nasimama na walimu kuwa waongezewe mshahara wao sasa. Kama si sasa ni sasa hivi. Walimu wamekuwa wakipigania haki yao ya nyongeza ya mishahara kwa muda mrefu. Naomba serikali iwaongezee mshahara wao kama njia mojawapo ya kuheshimu uamuzi wa mahakama,” alisema Namwamba.
Matamshi ya Namwamba yaliungwa mkono na wakazi wengi wa kaunti ya Nyamira, walimu wa kaunti hiyo wakiwa katika mstari wa mbele kwa kushikana kwa pamoja kuomba haki yao kutekelezwa mara moja ili kuendelea na masomo.
“Sioni haja ya kunyimwa haki yetu. Ni heri tuongezewe mshahara wetu ili tuendelee kufunza. Hapo mbeleni, mahakama kuu nchini iliagiza kuwa walimu waongezewe mshahara kwa asilimia 50 hadi 60 hadi sasa hatujaona pesa hizo,” alisema David Mokua, mwalimu.
Mgomo wa walimu unaendelea katika sehemu mbalimbali nchini huku wanafunzi wakienda shuleni kujifunza wenyewe.