Katibu mkuu katika chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Ababu Namwamba amewaomba vijana ambao wamehitimu umri wa miaka 18 kuchukua vitambulisho na kujiandikisha kama wapiga kura.
Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa Wakenya wengi ambao wametimu miaka 18 hawajajiandikisha kama wapiga kura nchini, jambo ambalo lilimlazimu Namwamba kuomba vijana na wananchi wote kwa ujumla kuchukua vitambulisho na kujiandikisha kama wapiga kura.
Kulingana na Namwamba, kujiandikisha ndio njia pekee ya kupata fursa ya kuwachagua viongozi wafaao ifikapo mwaka 2017 na hata kuwa na thibitisho kuwa mtu ni mwananchi.
Akizungumza siku ya Alhamisi katika eneo la Ekerenyo, wilayani Nyamira Kaskazini, alipokuwa anaendesha mradi wa 'Tokelezea ID’ wa kuwahimiza vijana kuchuwa vitambulisho kwa wingi, Namwamba alisema kura ndio silaha muhimu ya kuhakikisha viongozi wazuri wenye ndoto ya kufanya maendeleo wamechaguliwa.
Aliwaomba wale tayari wamechuwa vitambulisho kwenda mpaka ofisi za huduma kuchukua vitambulisho vyao.
Aidha, Namwamba aliongeza kuwa kujiandikisha kwa wingi huwa kunasaidia vijana kwa kujiunga kwa vyuo vikuu nchini, kutafuta kazi, kupanga ndoa na kukabidhiwa pesa za mikopo, haswa Uwezo Fund na zinginezo ili kufanyia biashara na kuinua uchumi na kujiimarisha kimaisha.
“Leo tumekuja hapa kwa nia moja pekee ya kuwahimiza vijana na wakenya kupata vitambulisho na kura. Nawaomba wakazi haswa vijana, kupata vitambulisho kwa wingi ili tuweze kuwachagua viongozi walio na maono ya kufanya maendeleo,” alisema Namwamba.
Wakati huo huo Namwamba aliwahimiza vijana wale walio na vitambulisho kuendelea kueneza habari ya kupasha wengine katika sehemu mbali mbali umuhimu wa kuchagua viongozi wa kutekeleza maendeleo kwa wananchi.