Baraza la makanisa nchini NCCK, linataka kaunti ambazo ziko katika maeneo ambayo hushuhudia visa vya kudorora kwa amani kutenga fedha za kutumika kuhubiri amani na upatanisho katika maeneo husika.
Katibu mkuu wa baraza hilo, kasisi Peter Karanja, alisema tangu kuanzishwa kwa mfumo wa ugatuzi nchini, kumeshuhudiwa mvutano kuhusu raslimali za mipakani.
Akihutubu mjini Eldoret katika chuo cha bibilia cha kanisa la Reformed church of East Africa siku ya Jumapili, Karanja alisema iwapo maswala ya amani na upatanisho katika kaunti kama hizo hayatapewa umuhimu unaostahili, huenda miradi za mabilioni ya pesa katika maeneo hayo zikasambaratika.
Kasisi Karanja alitaja kaunti za Nakuru, West Pokot, Turkana and Samburu kuwa miongoni mwa kaunti ambazo zimo hatarini iwapo maswala ya amani na upatanisho hayatapewa kipaumbele.
Kiongozi huyo alisema kuna haja ya kuhusisha vijana, wazee, viongozi wa kidini, akina mama miongoni mwa wadau wengine katika shughuli za kuhubiri amani ili kuhakikisha walengwa wanafurahia matunda ya ugatuzi.
Bw Karanja alisema malengo ya ugatuzi ya kuleta maendeleo mashinani yanapaswa kuhusisha wadau wote mashinani ili wajihisi kuwa sehemu ya maendeelo hayo na kuyalinda.
“Sijui ni kwa nini idadi kubwa ya kaunti ambazo zimo katika hatari ya kutokea kwa uhasama wa mipakani hazitengi pesa kwa ajili ya shughuli za amani na upatanisho," alisema Karanja.
Karanja alisema hakuna maendeleo yeyote ambayo yataafikiwa iwapo maswala ya amani hayatapewa umuhimu wa kwanza katika kaunti lengwa.
Wakati huo huo meja mstaafu John Seii alitaka kaunti zote humu nchini kushirikiana ili kuona kwamba kuna mazingira shwari ya amani kabla ya uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2017.
“Viongozi wa matabaka yote kutoka Rift Valley hawanabudi kuhubiri amani kabla ya uchaguzi mkuu ujao ikizingatiwa kuwa ghasia huzuka mara kwa wakati wa uchaguzi mkuu,” alisema Seii.