Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri ametuma pole kwa Mwakilishi wa Wadi ya Menengai Magharibi Lucy Nyambura Kihumba baada ya nyumba yake kuteketezwa akisema tukio hilo lilikuwa la kusikitisha.

Akizungumza katika hafla ya maombi ya kwanza ya Kaunti ya Nakuru yaliyofanyika wakati wa kiamsha kinywa siku ya Ijumaa, katika uwanja wa mkahawa wa Rify Valley sports club mjini Nakuru, Ngunjiri alisema ni jambo la kutia wasiwasi kwamba mwakilishi huyo aliteketezewa nyumba yake.

Ngunjiri amemtaka Gavana wa Kaunti ya Nakuru Kinuthia Mbugua kuandaa harambee ya kumsaidia mwaklilishi huyo wa wadi ili aweze kurejea katika hali yake ya kawaida.

“Nataka nitume pole kwa mwakilishi wa wadi ambaye alichomewa nyumba. Habari hiyo ilinigusa na nilisikia nikiwa na hofu sana kama tunaweza kumchomea mama kama huyo nyumba. Ni jambo la kuhuzunisha na tunafaa kuombea swala hilo. Gavana tuite harambee, tumjengee nyumba ili tumrudishe katika hali yake ya kawaida,” alisema Ngunjiri.

Kando na hayo, amemhimiza Gavana Mbugua kutia bidii kutatua matatizo yanayokumba kaunti hiyo na malumbano baina ya viongozi badala ya kusubiri kwa muda mrefu kabla ya kuwaita viongozi hao ili kujua ni tatizo gani lililopo.

Mbunge huyo alisema kuwa gavana ndiye kiongozi wa kaunti na kutokana na hilo, ana wajibu wa kufanya hivyo.

Pia amewataka viongozi kuwatumikia wananchi kwani walichaguliwa kufanya hivyo badala ya kuendeleza siasa zisizo na msingi.

Maombi hayo yalijumuisha viongozi kutoka sekta mbalimbali miogoni mwao akiwa Gavana Kinuthia Mbugua, Naibu Gavana Joseph Ruto, maseneta, wabunge, wawakilishi wa wadi, viongozi wa kidini, wafanyibiashara na wadau wengine kwenye Kaunti ya Nakuru.