Mbunge wa eneo bunge la Nyaribari Masaba kaunti ya Kisii Elijah Moindi amewashauri wakazi kutoka eneo bunge lake kuchukua pesa kutoka hazina ya fedha za vijana na wanawake ili wafanyie biashara badala ya kutegemea upikaji wa pombe.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu katika mji wa Kisii mbunge huyo alisema ili waweze kujitegemea na kuwa na maendeleo sharti watu wajiunge pamoja na kufanya biashara.
“Naomba watu wategemee biashara na ufugaji wa kuku na ng’ombe badala ya kuuza pombe haramu ambayo pia imegharimu maisha ya watu wengi hapa nchini na kusababisha hasara,” alisema.
Mbunge huyo aliongeza, “kutoka eneo langu naomba wananchi wakuje niwakabidhi pesa wafanyie biashara ili nao waweze kujikimu kimaisha kwa kufanya biashara mbalimbali kando na upikaji wa pombe.”
Aidha, Moindi aliwashauri wauzaji wa pombe haramu kutafta njia tofauti za kujipatia riziki badala ya kuendelea kufanya biashara ambayo ni kinyume cha sheria.
Wagema katika eneo hilo walisema kuwa wanategemea biashara hio kama njia ya pekee ya kulisha familia zao na kukimu mahitaji yao, jambo ambalo Moindi alisema sio la kweli. Alisema ni muhimu wabadilishe fikira zao.
“Hapo awali nilisema yeyote anayehitaji kufanya biashara akuje nimkabidhi pesa aanzishe biashara lakini wengi hawakutilia maanani, kwa sasa nawaomba waje niwape pesa waanzishe biashara,” alisisitiza.