Gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama amewataka wahudumu wa bodaboda kutoka kaunti hiyo kuwa na nidhamu na kielelezo chema kwa vijana wenzao.
Akiongea siku ya Ijumaa katika hafla moja ya kufungua taasisi ya fedha ya wahudumu hao wa bodaboda iliyopewa jina; Bondeni-Makairo Bodaboda Sacco katika eneo bunge la West Mugirango, Gavana Nyagarama alisema vijana wengi wanaouhudumu katika sekta ya bodaboda wamekuwa wakijihusisha na uhalifu na wengine kukosa maadili kwa abiria wao wanaowalaumu kwa kuwatusi watu barabarani.
Gavana huyo aliwasihi vijana hao waliokongamana katika hafla hiyo kubadilisha mienendo yao na wakati wote kujifundisha uhusiano mwema kupitia kwa wenzao na kufanya kazi yao tu kama kazi nyingine zile ambazo huwaheshimu wateja wao.
Ziadi ya yote, Nyagarama aliwataka vijana hao kujiepusha na kutumiwa vibaya na baadhi ya wanasiasa kwa kuzua fujo na kuandamana kupinga serikali yake, tabia aliyosema ni hatari kwa maendeleo ya kaunti hiyo.
Kwa upande wake, wakili Ben Mogaka ambaye ndiye mwanzilishi wa Sacco hiyo alisema kuwa kiini cha kuanzishwa kwa taasisi hiyo ni kuona kuwa vijana, sio tu wa bodaboda, bali vijana wote wanao ari na moyo wa kujiendeleza kiuchumi wana nafasi ya kuomba mikopo kutoka taasisi kama hizo ili kuinua uchumi.
Mogaka aliwashauri vijana wote wa kuendesha bodaboda kujiandikisha na Sacco hiyo ili iwe rahisi kwao kujipatia mikopo na kuweza kuendeleza biashara zao za bodaboda.
Pia aliwataka kuzitumia hela za mikopo kwa miradi zitakazowawezaesha kuzalisha maradufu na kuweza kuzirudisha kwa taasisi husika kwa wakati ufaao.