Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Seneta wa Nyamira Okong’o Omogeni ameitaka jamii ya Gusii kuzingatia wito wa rais wa Marekani Barrack Obama wa kuwapa watoto wa Kike nafasi maishani ili wajitegemee katika maisha ya baadaye na kujiepusha na mila za kale.

Seneta Okong’o, ambaye alikuwa akiongea katika mji wa Nyamira siku ya Jumatatu aliwaonya wazazi ambao wamekuwa na mazoea ya kutowapeleka watoto wa kike shuleni na kusingizia kuwa ni ukosefu wa karo, akiwaonya kuwa atapambana nao kupitia kwa taasisi za kisheria.

Aidha aliwataka wakazi kuwa katika mstari wa mbele kutoa ripoti iwapo dhuluma kama hiyo inaendelezwa na baadhi ya wazazi, si tu kaunti hiyo bali eneo la Gusii kwa jumla.

Kiongozi huyo pia aliwataka kina mama kuwa katika makundi mbali mbali ya kupigania haki zao ili iwe rahisi kuwasilisha malalamiko yao kupitia mashirika kama hayo, na kuwahakikishia kuwa siku zote atakuwa wa msaada mkubwa kwao iwapo watakumbana na vikwazo vyovyote wawe huru kumwambia.

Vilevile aliwataka viongozi wa vijiji, kata wakiwemo machifu na manaibu wao kutotishwa na yeyote wanapopiga vita tamaduni ambazo zimepitwa na wakati, akiwambia kuwa wao ni jicho la serikali na jamii.

Aliwataka vijana kufuata mazuri yaliyosemwa na Rais Barack Obama, na kamwe wasiwe wa kuiga tabia za nchi za magharibi kama vile ushoga kwa ni kinyume na maadili ya dini na maadili ya kiafrika.