Share news tips with us here at Hivisasa

Mkuu wa Idara ya afya katika Kaunti ya Mombasa amelitaka shirika la kupigana dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya nchini Nacada kujitolea kikamilifu ili kupigana na janga hilo.

Akiwahutubia wandishi wa habari mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Binti Omar alisema kuwa kuwa bado kuna kibarua kikubwa mbele yao na kuitaka halmashauri hiyo kutoa msaada wa kuwafadhili vijana zaidi kwenye kituo chao cha waathiriwa ambao wamejitolea kurekebisha tabia.

“Shirika la Nacada linahitaji kuwa katika mstari wa mbele kupigana na jinamizi hili na kuendelea kufadhili idadi kubwa, kuliko kuachia kaunti majukumu yote kwa sababu shirika hilo ndilo limepewa mamlaka ya kupigana dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya,” alisema Omar.

Omar alisema kuwa idadi ya vijana ambao wanahitajika kupewa msaada na kurekebisha mienendo ni wengi mno na itakuwa jambo la kuridhisha iwapo halmashauri hiyo itatoa ufadhili wa kifedha na kuongeza idadi ya vijana kwenye kituo chao.

Alisema kuwa serikali ya kaunti hata hivyo itakaza juhudi zake za kupigana na mihadarati na kuwa watakuwa na ari ya kusaidia wale ambao wanataka kujikwamua kutoka pingu za jinamizi hilo.

Alishtumu baadhi ya mienendo ambayo imekuwa ikijitokeza kwa baadhi ya waathiriwa kupatikana wakitumia dawa hizo kwenye vituo vyao vya kurekebisha tabia.