Share news tips with us here at Hivisasa

Gavana wa kaunti ya Kisii James ongwae amesema serikali ya kaunti hiyo imeweka mikakati kabambe ya kufungua kiwanda kipya cha maziwa mjini Kisii.

Akizungumza siku ya Ijumaa katika uwanja wa michezo wa Gusii alopokuwa amehughuria hafla ya maonyesho ya kilimo, Ongwae alisema kuwa serikali ya Kisii imejitayarisha kujenga kiwanda cha maziwa ili maziwa wakulima wanaofuga ng'ombe wa maziwa wanufaike.

Hii ni baada ya wakulima wengi kusema kuwa wanalazimika kuuza maziwa kwa bei ya chini sana na kuomba serikali ya kaunti hiyo kuwatafutia soko au jinsi ya kuhifadhi maziwa hayo.

”Tutahakikisha kiwanda cha maziwa kimejengwa hivi karibuni ili tutuze maziwa ya wakulima. Ninawaomba wakulima wote haswa wale wanaofuga ng’ombe wa maziwa wawe wakipeleka maziwa yao katika kiwanda hicho ujenzi utakapomalizika. Tutawalipa vizuri ili nao wafurahie matunda ya ufugaji,” alisema Ongwae.

Wakati huo huo, Ongwae alisema kiwanda cha parachichi kilichojengwa katika kaunti hiyo kitafunguliwa hivi karibuni baada ya kufungwa kwa muda.

Ongwae alisema kuwa serikali yake ya kaunti imetenga pesa za kuendeleza miradi ambayo itasaidia wakulima wa eneo hilo pamoja na wafugaji wa mifugo.

Aidha, Ongwae alisema kuwa kiwanda cha parachichi pindi kitakapofunguliwa kitaanza kutengeneza mafuta ya kujipaka.

"Fedha ambazo tutapata kutoka kwa mradi huo wa kutengeneza mafuta zitasaidia kuendeleza maendeleo katika kaunti hii ," alisema Ongwae.

Serikali ya Kaunti ya Kisii iliongoza kwa sekta ya kilimo katika utafiti uliofanywa na kampuni ya Infotrack huku Ongwae akiapa kuendelea na mtindo huo wa kuongoza katika sekta ya kilimo.