Gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae amepongeza maafisa wa polisi kwa kupunguza visa vya uhalifu katika kaunti hiyo.
Akizungumzaa siku ya Jumatano katika mkutano wa maafisa wa polisi na wakazi katika ukumbi wa kitamaduni mjini Kisii, Ongwae aliwapongeza maafisa wa polisi kwa juhudi ambazo wamekuwa wakifanya ili kupunguza visa vya uhalifu katika kaunti hiyo.
Ongwae alisema serikali yake ya kaunti itaendelea kufanya kazi pamoja na maafisa wa polisi ili kuhakikisha usalama kwa wananchi wa kaunti hiyo umeimarishwa.
“Naomba maafisa wa polisi kuendelea kuhakikisha usalama kwa wakazi wa kaunti yangu, nami kama gavana, nitaendelea kushirikiana nanyi ili tupunguze uhalifu zaidi,” alisema Gavana Ongwae.
Wakati huo huo, Gavana Ongwae aliwaomba wakazi wa kaunti hiyo kuripoti kisa chochote cha uhalifu punde tu watakapokishuhudia ili maafisa wa polisi waweze kulishughulia kwa haraka.
Ongawe alisema kuwa kunapaswa kuwa na ushirikiano kati ya maafisa wa polisi, wakazi na serikali ya kaunti ili kuhakikisha hakuna uhalifu katika kaunti hiyo.
Mkutano huo ulikuwa umepangwa ili kuwapa wakazi wa kaunti hiyo fursa ya kuwasilisha maoni yao kuhusu yale ambayo maafisa hao hawajashugulika kikamilifu.