Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae ameiomba serikali kuu kuweka ujenzi wa shule chini ya mamlaka ya serikali za kaunti kama njia moja ya kusaidia shule hizo.
Akiongea siku ya Jumapili katika hafla ya mchango wa kusaidia shule ya wavulana ya Nyamache, Ongwae alisema kuwa serikali kuu inastahili kupea serikali za kaunti mamlaka hayo ili ziweze kushughulikia masuala hayo kwa njia inayostahili ili kuinua viwango vya masomo katika kaunti zote nchini.
Ongwea alisema kuwa kuna changamoto nyingi ambazo zinatokea katika shule na zinahitaji usaidizi wa mapema ambao serikali ya kaunti inastahili kutoa ikipewa huo uwezo na vifaa vya kutoa huduma hizo.
“Serikali kuu inastahili kuweka mamlaka ya kushughulikia shule chini ya serikali ya kaunti kwani sisi ndio tuko karibu na shule hizo na tunajua yale yanahitajika kufanywa," alisema Gavana Ongwae.
Alitoa mfano wa upepo kubeba paa la shule au vyoo vya shule kuanguka huku akisema serikali za kaunti ndizo ziko karibu na zinaweza kutoa usaidizi wa haraka lakini hazina huo uwezo na pesa za kusaidia kwasababu mamlaka hayo yako chini ya serikali kuu.
Aidha, alisema kuwa serikali yake itaendelea kusaidia iwezalo katika sekta ya elimu ili kuinua viwango vya elimu katika shule zote za kaunti ya Kisii.
Ongwea alitoa mchango wake wa shillingi elfu 200 na kuwaomba wazazi, walimu na viongozi wote kushirikiana ili kuinua viwango vya elimu.