Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Serikali ya Kaunti ya Kisii imetoa orodha ya wafanyikazi wake ili waweze kujulikana.

Orodha hiyo ya wafanyikazi 5056 ilisomwa katika bunge la kaunti hiyo siku ya Jumatano na naibu wa kiongozi wa walio wengi katika bunge hilo Shem Ondara.

Orodha hiyo ilisomwa baada ya mwakilishi wa wadi ya Boochi Borabu, Samwel Onungo, kutaka wafanyikazi wote kujulikana ili kuonyesha uwazi kwa wakazi wa kaunti hiyo.

Kulingana na orodha hiyo, wafanyikazi wa kiume walikuwa 2409 huku wafanykazi wa kike wakiwa 2647.

Wakati huo huo, miongoni mwa wadi 45 ambazo ziko katika kaunti ya Kisii wadi ya Kisii ya kati ndio inaongoza kwa kuwa na wafanyikazi wengi zaidi kuliko wadi zote.

Wadi hiyo ina wafanyikazi 205 huku wadi ya Boochi Borabu iliyo na wafanyikazi 45, ikiwa wadi iliyo na wafanyikazi wachache zaidi.

Jambo hilo liliweza kuibua hisia tofauti katika bunge hilo kwani wadi ya Monyerero, Nyakoe, Masimba na ile ya Kiogoro, hazikuwa na wafanyikazi wowote katika orodha hiyo.

Mwakilishi Ondara aliomba muda zaidi wa kuorodhesha vizuri wafanyikazi wa kaunti na wadi wanazozitoka, majina yao kamili na lini waliajiriwa ili kuonyesha uwazi.

Spika wa bunge la kaunti hiyo Okerosi Ondieki alikubaliana na Ombi hilo na kumpa Ondara siku 14 kufanya hivyo.

Aidha, ripoti hiyo ilionyesha bunge la kaunti hiyo inamiliki wafanyikazi 116 badala ya kuwa na wafanyikazi 54.