Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Afisa moja wa polisi na mfanyi kazi mmoja wa shirika la nguvu za umeme nchini KPLC wamekamatwa na maafisa wa tume ya kukabiliana na ufisadi nchini kwa tuhuma za kuhusika katika ufisadi.

Tukio hilo lilitokea siku ya Jumanne katika eneo la kambi ya Moto katika jimbo la Nakuru.

Wawili hao, Inspekta Peter Wambua na James Michuki ambae anahudumu na shirika hilo kama fundi wa mitambo wanadaiwa kushirikiana kwa pamoja katika kuwalaghai wakazi wa Nakuru kutoka sehemu mbali mbali.

Wawili hao wanadaiwa kuwaunganishia wakazi umeme kinyume na sheria.

Katika operesheni hio, kiasi cha pesa shillingi 150,000 kilipatikana kutoka kwa wawili hao na inaaminika kuwa ni kati ya pesa ambazo walizipokea kutoka kwa wakazi kwa njia isiyo halali.

Kaimu mkurugenzi wa tume ya kupambana na ufisadi katika eneo la Kusini Mwa Bonde la Ufa Bwana Gilbert Lukhoba alisema kwamba wawili hao walipatikana katika harakati za kukusanya pesa kwa wateja wa shirika hilo la umeme.

“Tulipokea taarifa kwamba kuna ulaghai uliokuwa ukiendeshwa na wawili hawa na ndio tukaanza operesheni ya kuwatafuta na kweli tumewapata wakikusanya pesa,” alisema Lukhoba.

Alisema wawili hao walipelekwa katika kituo cha polisi cha Central mjini Nakuru ambako watazuiliwa huku uchunguzi ukiendeshwa.

Kaimu mkurugenzi huyo pia amewahimiza wananchi kushirikiana nao katika kuhakikisha kwamba visa kama hivyo vinafikia kikomo.

“Tunawahimiza wananchi waendelee kushirikiana nasi kwa kupiga ripoti kuhusu visa kama hivi ili kwa pamoja tukomeshe uhalifu huu," alisema Lukhoba.