Share news tips with us here at Hivisasa

Maafisa wa polisi mjini Mombasa wamepinga madai ya kuhusika na visa vya mauaji na kupotea kwa vijana mara kwa mara kutokana na kushukiwa kuwa wafuasi wa wanamgambo wa al-Shabab.

Kamanda mkuu wa Polisi katika Kaunti ya Mombasa Francis Wanjohi alisema kwamba kamwe maafisa wa polisi hawajahusika na vitendo kama hivyo huku akishikilia kwamba huenda kuna watu fulani walihusika kuwateka vijana hao nyara ama kuwaua kwa sababu zisizoeleweka.

Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatano, Wanjohi aliwataka wakazi kutoa habari muhimu kuhusu washukiwa wanaodaiwa kuhusika na kuwateka vijana hao nyara kwani maafisa wa polisi wanao watia nguvuni vijana huwazuilia katika kituo cha polisi na baadaye huwafikisha mahakamani.

Aidha, alitoa hakikisho kwa wakazi kuwa kwa sasa hakuna vijana kama hao wanazuiliwa katika vituo vya polisi mjini Mombasa, licha ya idara hiyo ya usalama kuanzisha uchugunzi wa kina kubaini madai yanayotajwa na baadhi ya familia mjini humo kwamba maafisa wa polisi walihusika kuwateka vijana hao nyara.

“Hakuna afisa yoyote wa polisi aliwahi husika katika kuwaua vijana wala kuwateka nyara bila sababu zozote mwafaka za kushukiwa na uhalifi ama ugaidi. Tumeanzisha uchunguzi kubaini madai hayo na endapo wako maafisa wa polisi wanaohusika basi hatua za kisheria zitachukuliwa,” alisema Wanjohi.

Aidha, alidokeza kuwa maafisa hao wanawasaka baadhi ya vijana wanaodaiwa kuwa wahalifu katika Kaunti ya Mombasa na eneo la pwani kwa jumla na endapo watawatia nguvuni, basi watafunguliwa mashtaka.

Haya yamejiri siku moja tu baada ya familia katika eneo la Bondeni mjini Mombasa kulalamikia haki zao baada ya kudai kuwa maafisa wa polisi walihusika katika kutoweka kwa jamaa wao.