Share news tips with us here at Hivisasa

Maafisa wa polisi wa kituo cha Nyamira wameanzisha uchungunzi wa kuwatafuta washukiwa wawili wa uhalifu ambao walishambulia kituo kimoja cha kuuza mafuta cha National Oil kilichoko katika mji wa Nyamira na kuiba Sh600,000.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu mjini Nyamira, mkuu wa polisi wilayani Nyamira Ricah Ongare alisema washukiwa hao wa uhalifu waliokuwa na bunduki walimwagiza mfanyikazi mmoja wa kituo hicho cha mafuta kuwaonyesha afisi ya meneja, walipoenda na kumtishia meneja huyo na kisha kuiba pesa hizo.

Hata hivyo, Ongare alisema kisa hicho ni cha kushangaza mno kwani pesa za kituo hicho cha mafuta hupelekwa kwa benki kila siku huku ikisemekana kuwa kwa siku tatu zilizopita, pesa hizo hazikuwa zimepelekwa benki.

“Uchunguzi umeanzishwa kubaini uwazi wa wizi huu kwani washukiwa hao walikuwa na bunduki walipomfahamia meneja,” alisema Ongare.

Visa vya uhalifu vimekuwa vikiongezeka katika kaunti ya Nyamira kwa siku za hivi majuzi.

Siku ya Jumapili, ajuza mmoja kutoka kijiji cha Bochari kaunti ya Nyamira mwenye umri wa miaka 72 aliuawa na watu wasiojulikana baada ya genge hilo kuvamia boma ya mwanamke huyo anayeishi na mjukuu wake.