Gavana wa Kaunti ya Lamu Issa Timamy imeitaka idara ya polisi kuzidisha juhudi zake za kuimarisha usalama katika barabara kuu ya kutoka Lamu hadi mjini Mombasa.
Kulingana na Timamy, wakazi wanaotumia barabara hiyo huhofia usalama wao kutokana na tetesi kuwa huenda kuna watu fulani wanaolenga kuyavamia mabasi ya uchukuzi wa umma.
Akizungumza na wanahabari katika Makavazi ya Fort Jesus mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Timamy alisema kwamba lazima usalama uimarishwe kikamilifu kwa wakazi sambamba na wale wanaosafiri ili kuepukana na visa vya uvamizi ambavyo huchangia maafa kwa wakazi wasio kuwa na hatia.
Aidha, alipendekeza mpango wa mabasi hayo ya uchukuzi wa umma kusafiri na maafisa wa polisi ili kuwapa abiria usalama dhabiti na kuwaondolea hofu ya ukosefu wa usalama katika barabara hiyo.
“Tungependa idara ya polisi kuanzisha mpango wa kuweka maafisa wao katika mabasi hayo na kusafiri moja kwa moja na abiri ili kuimarisha usalama na kudhibiti visa vya uvamizi wa mabasi ya abiri na wahalifu,” alisema Timamy.
Timamy alishikiza kusitishwa kwa safari za usiku na akasema kwamba safari hizo zinachangia kukithiri kwa visa vya uvamizi huku akivitaka vitengo mbalimbali vya maafisa wa usalama kushirikiana na wakazi kudumisha usalama.