Baadhi ya wakaazi wa mji wa Kisii wameitaka idara ya polisi kuanza kushika doria na kufunga baadhi ya maduka na majumba ya kuuza pombe haramu.
Wakaazi hao wamewalaumu baadhi ya maafisa hao kuwa wao ni kikwazo kikubwa katika vita dhidi ya unywaji wa pombe haramu na matumizi ya dawa za kulevya katika kaunti hiyo.
Wakiongozwa siku ya Jumapili na mmoja wa viongozi wa wafanyibiashara kutoka mji huo, Gilbert Mochoge, wakaazi hao walisema kuwa maduka ya kuuza vileo katika eneo hilo hayana vibali vya kibiashara na kuendeleza shughuli hizo.
Walisema kuwa vijana wengi, wamekuwa wakijihusisha na unywaji wa pombe kupita viwango vinavyofaa na kujijipata wamelala kando ya barabara na vichorochoroni hasa nyakati za wikendi.
Bwana Mochoge hakusita kuwatia dosari baadhi ya maafisa hao wa polisi ambao wamekuwa wakizunguka katika majengo ya kuuza vileo aina mbali mbali.
Alidai kuwa polisi hao wanachukua hongo ili kuwapatia wauzaji nafasi na kuuza pombe ambayo imepigwa marufuku na halmashauri ya Kupigana na Unywaji pombe na Matumizi ya Dawa za Kulevya nchini NACADA.
Haya yanajiri siku mbili tu baada ya kijana mmoja anayedaiwa kuwa mwanafunzi wa chuo kikuu kunywa pombe na kunusurika kifo alipookolewa kwa kupewa maziwa na polisi na wapita njia.
Mji wa kisii umeshuhudia visa vya unywaji pombe haramu na utumizi wa dawa za kulevya huku ikisemekana kuwa idadi kubwa ya vijana hususan wale waliomo vyuoni hushawishiana kwenye uraibu huo.