Maafisa wa polisi eneo la Joska, kaunti ndogo ya Matungulu katika kaunti ya Machakos wanamsaka mwanamume mmoja aliyemkata mkewe sehemu za siri na kutoweka siku ya Jumamosi.
Mwanamke huyo anaendelea kuuguza majeraha katika hospitali ya Mama Lucy huku mumewe akiwa mafichoni.
Akidhibitisha kisa hiki cha kushangaza afisa mkuu wa Matungulu Bwana Joseph Chesori alisema kuwa mwanamume huyu alitekeleza uovu huo mkewe alipokuwa amelala, baada ya kumfumania kwenye klabu na mwanamume mwingine.
Vilevile alielezea kuwa uchunguzi umeanzishwa kubaini ukweli wa mambo na kumsaka mshukiwa.
"Visa kama hivi havijaripotiwa kwa muda mrefu lakini tumeanzisha uchunguzi kubaini ukweli wa kisa hiki," alisema Chesori.
Afisaa huyo pia alimwomba mshukiwa kujisalimisha kwenye kituo cha polisi kilicho karibu ili kurahisisha mambo.
"Ingekuwa vyema mshukiwa huyo angejisalimisha kwa mikono ya polisi kwa usalama wake na pia kujirahisishia mambo," aliongezea Chesori.
Wananchi pia waliombwa kushtaki kwenye kituo cha polisi kilicho karibu iwapo wangejua alipo mshukiwa.