Maafisa wa polisi wameombwa kuwasaka na kuwatia mbaroni wezi wa ng’ombe ambao wanaendelea kutekeleza wizi huo kila mara katika eneo la Isoge, eneo bunge la Borabu, Kaunti ya Nyamira.
Wito huo umetolewa baada ya wizi wa ng'ombe kuendelea kuongezeka kila mara katika eneo hilo jambo ambalo limeonekana kuwa la kawaida.
Akizungumza katika eneo la Borabu siku ya Jumapili, wakili Yobesh Kambi aliwaomba maafisa wa polisi kujaribu kila wawezalo ili kuwatia mbaroni wanaotekeleza wizi wa ng’ombe katika eneo hilo.
“Naomba maafisa wa polisi kuwasaka na kuwatia mbaroni wezi wanaondelea kuiba ng’ombe katika eneo la Isoge,” alisema Kambi.
Aliongeza, “Maafisa wa polisi wanapaswa kuwatia mbaroni wezi hao wafikishwe mahakamani na kufunguliwa mashtaka ya wizi na kuchukuliwa hatua kali ya kisheria, kwani wizi wa aina hii umekuwa ukiongezeka kila mara katika eneo hili.”
Aidha, Kambi aliwaomba wakazi kushirikiana na maafisa wa polisi kuwasaka wezi hao.
Wakazi walisema nyumba nyingi huvunjwa wakati wa usiku na ng'ombe huendelea kuibwa huku wakisema wamekuwa wakipiga ripoti kwa polisi lakini hamna hatua imechukuliwa hadi sasa jambo ambalo limewaacha wengi vinywa wazi.
Pia Wakazi hao wamewaomba machifu kushirikiana pamoja na maafisa wa utawala kuzuia wizi wa aina hiyo ambayo unaendelea kuongezeka kila mara.
“Mie naona tukiungana pamoja sisi sote na tuwe na umoja, wizi wa ng’ombe katika eneo hili hautaendelezwa. Tunastahili tushikane mikono tupambane na wizi huu ili tusishuhudie wizi wa aina hii tena katika eneo letu la Borabu Isoge,” alisema Shadrack Mainga, mkazi.