Share news tips with us here at Hivisasa

Tume ya kuajiri walimu nchini TSC, tawi la Mombasa imesema kuwa mitihani ya kitaifa ya darasa la nane na kidato cha nne itaendelea kama ilivyoratibiwa.

Kwenye mkao na wanahaabri mjini Mombasa katika afisi za tume hiyo siku ya Jumatano, mkurugenzi wa tume hiyo Kaunti ya Mombasa, Ibrahim Rugut, alisema kwamba mitihani ya kitaifa itakafanyika bila pingamizi zozote licha ya walimu kushiriki mgomo iliyotajwa kuwa sio halali.

Rugut alisema kwamba Wizara ya Elimu inapanga mikakati mwafaka ya kufanikisha shughuli za masomo na mitihani ya kitaifa inafanyika vyema kwani wanafunzi wamejitayarisha vyema na lazima watafanya vyema katika mitihani hiyo.

“Mitihani ya kitaifa ya darasa la nane na kidato cha nne itafanyika kama ilivyoratibiwa hata walimu wasiporudi shuleni. Wizara ya Elimu imepanga mikakati mwafaka ya kushughulikia masomo na mitihani ya kitaifa na tuna matumaini kuwa wanafunzi mwaka huu watafanya vyema,” alisema Rugut.

Aidha, alisema kwamba mgomo wa walimu kote nchini unafaa kusitishwa mara moja kwani sio halali na viongozi wa vyama vya walimu Knut na Kuppet wanamalengo potovu kwa wanafunzi na walimu, kwani huwatetea walimu ili kujibinafsisha wenyewe na wala sio kuimarisha viwango vya elimu.

Rugut alishikilia kwamba iwapo walimu wataendelea kushiriki mgomo usio halali, basi wataadhibiwa kwani mgomo huo mahakama umesema wazi kuwa sio halali kutokana na vyama hivyo kukosa kuwasilisha barua ya notisi ya siku 14 kabla ya walimu kushiriki mgomo.

“Viongozi wa vyama vya walimu nchini Knut na Kuppet wanamalengo potovu kwa sababu sheria inasema wazi kuwa lazima utoe notisi ya siku 14 kabla ya kushiriki mgomo. Hawa viongozi wa walimu wanamalengo ya kujinufaisha wenyewe wala sio kutetea walimu,” aliongeza Rugut.

Mkurugenzi huyo wa TSC kaunti ya Mombasa amezidi kuwatahadharisha walimu watakaokosa kufika shuleni baada ya kukamilika kwa siku 14 wataadhibiwa na kufurushwa kazini.