Share news tips with us here at Hivisasa

Seneta wa Kaunti ya Nyamira Kennedy Okong’o ameahidi kuendelea kusaidia hospitali zilizoko katika kaunti hiyo kwa kuzinunulia dawa za matibabu ili kuboresha huduma za matibabu.

Akizungumza siku ya Jumapili katika hospitali ya Riomego ilioko eneo bunge la Mugirango Kaskazini, seneta huyo alisema kuwa yeye kama kiongonzi wa kaunti hiyo ataendelea na usaidizi wake kwa kununulia hospitali za kaunti hiyo dawa ya kutibu magonjwa mbali mbali ili wakaazi wa eneo hilo haswa wagonjwa waweze kufaidika na huduma bora katika hospitali ya kaunti hiyo.

Hii ni baada ya hospitali nyingi katika Kaunti ya Nyamira kuonekana kutokuwa na dawa za kutosha, jambo ambalo lilimpelekea seneta Okong'o kuanzisha mradi huo wa kununua dawa.

"Ninaona watu husumbuka sana haswa wanapotafuta huduma za matibabu wanapoenda katika baadhi ya hospitali za kaunti hii na wanakosa dawa," alisema Okong’o.

Seneta Okong'o aliongeza kuwa wagonjwa huwa wanaenda kwa hospitali kisha wanatumwa kwa zahanati zingine tofauti kutafuta dawa kwa sababu ya kukosekana kwa dawa kwenye baadhi ya hospitai Nyamira.

"Wakaazi wa Nyamira wanastahili kuhudumiwa kikamilifu katika hospiatali za kaunti hii, ndio maana nimeanzisha mradi wa kununulia hospitali za kaunti hii dawa kwa pesa zangu binafsi," aliongeza Okong’o.

Kwa upande mwingine, wakaazi wa kaunti hiyo walifurahishwa na seneta huyo na kumshukuru kwa kuamua kuwasaidia kwani wamekuwa wakisumbuka kutafuta dawa ili kutibiwa.

"Tunasema asante kwa seneta wetu kwa kuamua kusaidia hospiatali za kaunti hii kwa kununua dawa za matibabu. Tungekuwa na viongonzi kama hawa, basi hatungekuwa na shida kamwe katika kaunti yetu haswa ya kukosekana kwa dawa za matibabu," alisema John Omwanza mkaazi.

"Tunawaomba viongonzi wengine tuliowachagua kushirikiana na seneta wetu kwa kutoa msaada huu ili hospiatali zetu ziwe na dawa za kutosha," alihoji Peterson Omariba, mkaazi mwingine.