Seneta wa Kaunti ya Nyamira Kennedy Okong’o amewaomba madaktari wanaohudumu katika hospitali za hiyo kuwajibika vilivyo kwa kazi wanayoifanya.
Hii ni baada ya daktari mmoja kuthibitisha kuwa mtoto amefariki ilhali bado alikua hai.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Alhamisi katika mji wa Nyamira, Seneta Okong’o alisema ikiwa madaktari hawatafanya kazi yao vilivyo, watachukuliwe hatua kali za kisheria pamoja na kusimamishwa kazi.
Aidha, seneta aliomba madaktari waweze kuwajibikia kazi yao jinsi walivyopokea mafunzo wakati walipokuwa katika vyuo ili kutoleta maneno ya kutatanisha kwa wagonjwa wale ambao wamelazwa hospitalini.
Seneta Okong’o alidai anayesimamia idara ya afya katika Kaunti ya Nyamira Andrew Ombati anastahili kusimamishwa kazi kwa kutowajibika katika wizara yake ya afya kikamilifu.
“Anayesimamia idara ya afya katika Kaunti ya Nyamira anastahili kusimamishwa kazi maana angewajibika kwanza kabla ya madktari kusema mtoto amekufa ilhali alikuwa hai,” alisema Okong’o.
Wakazi wa kaunti hiyo walishangazwa na kisa hicho huku wengi wakisema wanahofia maisha yao kwani wanapowapeleka wagonjwa hospitalini mgonjwa anaweza kuwa hai lakini athibitishwe kuwa amefariki.
“Mimi mwenyewe nimepoteza imani kwa madaktari wa kaunti yetu maana wameanza unjanja kwa kusema mgonjwa amekufa na hajakufa,” alisema Albert Nyamwamu, mkazi.
“Tunaomba kuanzia leo wakati daktari anaposema jambo lolote ambalo ni kinyume na mgonjwa achukuliwe hatua ya kisheria,” alisema Brenda Bosibori, mkazi.