Baada ya visa vya ajali kuzidi kuongezeka katika soko la Daraja Mbili, wafanyibiashara kwa soko hilo wameiomba serikali ya kaunti kuwajengea kivukio cha juu ili kupunguza ajali za barabara katika eneo hilo.
Ombi hilo limetolewa kwa serikali ili kuingilia kati na kutatua changamoto wafanyibiashara wa soko la Daraja Mbili hupitia wakiendelea na mauzo yao hasa siku za soko.
kulingana na wafanyibiashara hao, watu wengi hugongwa na magari yanayoleta msongamano mkubwa na kuendeshwa kwa kasi katika barabara inayopita katikati mwa soko hilo kila siku ya Jumatatu na Alhamisi ambapo siku hizo ni siku za soko hilo.
Wakizungumza Jumatatu katika soko hilo, wafanyibiashara hao wakiongozwa na Lilian Omweri walisema watu hujeruhiwa na magari yanayoendeshwa kwa kasi.
“Wiki jana siku ya Alhamisi gari lilinigonga kwa bahati halikuwa linaendeshwa kwa kasi sana. Naomba serikali isikie kilio chetu ili maisha yetu yasiwe hatarini kila wakati na kujenga kivukio hicho ili tuwe tunavuka kutoka ng’ambo ingine kuelekea ingine tukitumia kivukio,” alisema Daniel Mikae, muuza begi katika soko hilo.
“Naomba tujengewe kivukio hapa iwe rahisi kwetu kuvuka kuelekea ng’ambo ingine,”alisema Zipporah Osoro muuza nyanya.