Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Watu wanaoishi na ulamavu katika Kaunti ya Nyamira wameiomba serikali ya kaunti hiyo kuhakikisha kwamba shughuli yakujengwa kwa maktaba ya umma kwenye kaunti hiyo inaharakishwa ili kuwasaidia wanafunzi kusoma.

Wakiongea na wanahabari mjini Nyamira siku ya Ijumaa, walemavu hao waliomba serikali ya kaunti hiyo kuhakikisha kuwa maktaba hiyo imejengwa haraka ili kukidhi mahitaji ya wananchi.

Kulingana Bw Japhet Mang'aa, asiye na uwezo wa kuona, watu wanaoishi na ulemavu katika kaunti hiyo walikuwa wameiomba serikali ya kaunti kujenga maktaba hali iliyosababisha bunge la kaunti kutenga pesa zakufadhili mradi huo na sasa wanashindwa mbona bado serikali hiyo inajikokota kutekeleza swala hilo.

"Tulikuwa tumeiomba serikali ya kaunti kujenga maktaba ya umma swala ambalo bunge la kaunti lilichangamkia kwa kutenga pesa zakufadhili mradi huo kwenye makadirio yao ya bajeti. Sasa tunashindwa mbona serikali ya kaunti inaendelea kujikokota kutekeleza mradi huo,” alisema Mang'aa.

Mang'aa aidha ameongeza kwa kuiomba serikali ya kaunti hiyo kuhakikisha kwamba kuna vitabu spesheli vya 'brail' ili kuwasaidia wasio na uwezo wa kuona kusoma kwa urahisi.

Mang'aa aidha alichukuwa fursa hiyo kuiomba serikali ya kaunti hiyo kuhakikisha kwamba asilimia 30% za kandarasi zinatengewa vijana, kina mama na watu wanaoishi na ulemavu kwa mujibu wa katiba kwa kuwa ni haki.

Kundi hilo la watu wanaoishi na ulemavu aidha waliomba serikali ya kaunti ya Nyamira kuwatengea asilimia tano ya nafasi za ajira huku wakisihi kamishna wa kaunti hiyo Bi Josphine Onunga kuhakikisha kuwa afisi zote za serikali ziko katika hali nzuri yakuwahimili walemavu.