Idara ya usalama na ile ya kudhibiti shughuli za barabarani katika Kaunti ya Kisii imetakiwa kukomesha utoaji rushwa na kuweka utaratibu mwafaka wa kulipia vibandiko.
Akizungumza siku ya Jumanne katika ofisi ya kaunti wakati wa kuondosha pikipiki zilizoshikwa na kufungiwa na askari wa kaunti katika makao makuu ya ofisi ya kaunti, mwenyekiti wa steji ya Mashauri Charles Ogega, aliwasuta maafisa wa kaunti ambao uhudumu kama askari katika barabara kuu ya kutoka mjini Kisii kuelekea Kilgoris kwa kuwadhulumu waendeshaji bodaboda.
"Askari hao wamekuwa wakiwashika waendeshaji bodaboda hata wakati wamelipia vibandiko na baadaye kuwanyanganya na kuzuilia pikipiki zao. Hali hiyo imekuwa kama mtindo miongoni mwa askari hao," alisema Ogega.
Aidha, alisema kuwa wengi wa waendeshaji bodaboda wameumizwa kwa kupigwa na askari hao wanapokuwa wakitetea haki yao na kuwalaumu wengine kwa kutaka kuhongwa ili waachilie pikipiki zao zinapozuiliwa.
Ogega aliitaka serikali ya kaunti kupitia Wizara ya Mpangilio wa Mji na ile ya Uchukuzi katika Kaunti ya Kisii kutafuta suluhu la haraka.
Mwenyekiti huyo alitishia kuwa waendeshaji bodaboda watafanya maandamano iwapo askari hao wataendelea kuwadhulumu.
Haya yanajiri baada ya wahudumu wa magari aina ya Probox kufanya maandamano wakilalamikia kudhulumiwa na askari hao.