Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakazi Mombasa wameitaka serikali ya kaunti hiyo kuwahamisha watoto wanaorandaranda mtaani kutoka mji huo na kuwaweka katika nyumba za watoto.

Wakazi hao walisema kuwa watoto hao ndio wamechangia kudorora kwa usalama nyakati za usiku katika jiji hilo na kutishia kuchukua hatua ya kuwafurusha watoto hao iwapo hatua ya haraka haitachukuliwa.

Wakazi hao kutoka maneo ya makazi ya Ganjoni, Kizingo, eneo la Docks na maeneo mengine yanayozunguka mji huo, walisema kuwa vijana hao wamekuwa na mazoea ya kuwashambulia watu nyakati za asubuhi na nyakati za usiku ambapo huwaibia na hata kuwapiga vibaya.

Wakiongozwa na mwanaharakati wa haki za binadamu na masuala ya jamii Bwana Salim Mwinyi siku ya Jumapili katika kikao cha kujadili masuala yanayowaathiri wakazi, walisema kuwa serikali kuu imeshindwa kushughulikia watoto hao wa mtaa na huenda mzozo ukazuka, ikizingatiwa kuwa jamii hiyo ya mtaa inaendelea kukua kila mara kwa kuzaana na wengine kuletwa na wazazi ambao wameshindwa na majukumu ya kulea watoto.

Mwinyi aliitaka serikali ya kaunti kutafuta mbinu mwafaka ya kuwatoa watoto hao mtaani na kuwapeleka kwenye nyumba za watoto, na wengine kutafutiwa makwao.

Alisema kuwa baadhi ya watoto wa mtaa wana familia na huenda wengine wametoroka kwa sababu ya malezi mabaya kutoka kwenye wazazi wao.

“Wajibu ni wetu kama jamii kuona kuwa tunafaana kwa kuwapa njia mwafaka watoto hawa wa mtaa. Si vizuri kaunti ikae na kupuuza swala hili kama serikali kuu imeshindwa kulitatua. Sharti tuwajibikie malengo ya kuwafaa wale ambao tunawaongoza,” alisema Mwinyi.