Share news tips with us here at Hivisasa

Seneta wa kaunti ya Kisii Christober Obure ameomba serikali ya Kaunti ya Kisii kununua mashine ya kuosha vitambaa vya wagonjwa katika hospitali ya Gucha iliyoko eneo bunge la Bobasi.

Wito huo umetolewa baada ya seneta Obure kutembelea hospitali hiyo bila kutarajiwa na kupata jinsi vitambaa vya wagonjwa huoshwa katika hospitali hiyo, shughuli ambayo haikumfurahisha na kusema wale wa kuosha vitambaa hivyo wanaweza ambukizwa magonjwa ya kila aina.

Hali hiyo ilimlazimu kumuomba Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae kulitafutia suluhu ya haraka.

Aidha, seneta Obure alisema chumba ambacho kinatumiwa kwa kupika chakula siyo kizuri na kusema ni cha zamani mno na kuomba kirekebishwe kwani hospitali hiyo ni kubwa zaidi na ni ya pili katika Kaunti ya Kisii, na kwa hiyo inafaa iwe na mazingira masafi.

“Chumba kile kinachotumika kama jikoni ni cha zamani sana kinastahiIi kubadilishwa na serikali ya Kaunti ili kiweze kuwa mpya na kuhakikishia mazingira mema katika hospitali hii ya Gucha," aliongezea Obure.

Aliyasema haya yote siku ya Jumatatu katika hospitali hiyo alipoizuru kighafla.

Kwa upande wake, daktari mkuu katika hospitali hiyo Bw Charles Ayora alisema kuna upungufu wa madaktari katika hospitali hiyo na kumuomba Gavana Ongwae kuwaongeza madaktari ili huduma ziweze kuimarishwa katika hospitali hiyo.

Seneta Obure pia alisema hospitali zote katika Kaunti ya Kisii ziongezewe dawa za kutosha huku hospitali ya Gucha ikiwa moja wapo.